“Ipo siku nitatoboa”huu ni msemo wa vijana wengi mtaani ambao kila kukicha huamka asubuhi na kuanza kufukuzia ndoto zao kwa kufanya kazi mbalimbali ili kujikimu kimaisha,msemo huu wa kutoboa haumaanishi kutoboa sufuria,nguo,ukuta au suruari,bali kuwa na maisha mazuri yenye utele kifedha na inayoweza kusababisha kaka zako wakakuita baba,mama yako akajivunia uwepo wako duniani.
Maana halisi ya kutoboa ni kukifanya kitu kuwa na tundu hivyo kuleta urahisi wa kupenyeza kitu,kupita au kupitisha kuchungulia mahali.Pamoja kuwa kutoboa ni lugha isiyo rasmi lakini inamaanisha kufanikiwa kimaisha vilevile ina maana kuntu kuwa kutoboa kitu sio mchezo wala lelemama ni lazima uwe na kisu,nyembe panga kali,bludoza,nyundo nk.
Watu wengi wamekuwa wakijidanganya kuwa watatoboa kiurahisi hali ambayo wamekuwa wakifanya vitu kirahisi rahisi,au wanachukulia poapoa au simposimpo vile wenyewe wanasema kiulaniniii.Mara nyingi aina ya watu hawa wanashindwa kutoboa hali ambayo inawaacha na maswali mengi.Unafikiri tatizo la watu hawa ni nini?Vifaa wanavyotobolea ni butu,vyepesi au wepesi wa kukata tamaa vipi kuhusu nyota?
Kama unataka kutoboa haina haja ya kujiuliza juu ya ubutu wa kifaa chako,ung’aro wa nyota yako,bali una haja ya kujiuliza ni njia gani sahihi unapaswa kutumia ili kutoboa kwa usahihi?Hahaaa msomaji wangu jibu ni hili hapa.
1.KUWA NA MALENGO
Kitendo cha kutoboa huwa hakifanyiki peke yake,lazima kunakuwa na muunganiko wa vitu vingi kama Nguvu za Mtoboaji,kitu kinachotobolewa,kifaa cha kutobolea na unatoboa kwa lengo gani.
Watu wengi wameshindwa kutoboa kwa sababu ya kukosa lengo hasa linalowafanya kutoboa,wamekuwa wakitoboa ukuta,bati bila ya kuwa na nyenzo thabiti ya utoboaji.
Kila mtoboaji anapaswa kuwa na lengo,mfano anayetoboa bati ana lengo la kutoboa ili agonge msumali na kuezeka nyumba na nyenzo zake ni nyundo na msumali.Sasa katika maisha halisi ni kuwa unapaswa kuwa na malengo ambayo yatakufikisha mahali unapopataka.
JINSI YA KUWEKA MALENGO
Malengo ni nadharia,au ni imani anayotengenezwa katika jambo Fulani ambalo kwa baada ya wiki,mwezi,mwaka,miaka kadhaa linaweza kuwa halisi,kujiwekea malengo ni hatua ya kwanza ya kufanya visivyoonekana vionekane.
Maisha bila ya malengo ni sawa na kuanza safari bila kujua unakwenda wapi.
Malengo ni ramani ya barabara inayoongoza na kukuonyesha ni kitu gani ambacho unahitaji kufanya katika maisha yako,kuna aina mbili za malengo ambazo ni malengo ya muda mfupi na malengo ya Muda mrefu.Malengo haya yanaweza kuwa ya siku,wiki,mwezi,mwaka hata miaka 50.
Unapoianza siku anza kwa malengo
Kila unapoianza siku unapaswa kuwa na malengo ya siku hiyo, ni lazima uwe na orodha muhimu ambayo itakuongoza siku hiyo,ni orodha muhimu ambayo itakuwa na mwongozo wako kwa siku nzima.
Unapoianza siku yako unapaswa kutafakari kwa kina ni matokeo yapi unataka kuyapata kwa siku hiyo.Epuka kuianza siku kwa bahati mbaya,anza siku yako ikiwa imepangiliwa vizuri ili uweze kupata matokeo chanya katika siku yako hiyo.
Ni muhimu kuwa na malengo ya muda mrefu ambayo unayafanyia kazi kila siku,kwani mafanikio ni mkusanyiko wa siku mbalimbali ambazo umeishi kwa malengo na kufanya kazi kwa bidii.
Ili kutimiza malengo yako inakupasa kukaa mbali na watu wenye fikra hasi,watu hawa wanaweza kukatisha tama,unaweza sikia maneno
“Alishindwa flani ambaye ana pesa utaweza wewe”Haupaswi kusikiliza sauti,tena mara nyingine waambie kabisa kuwa una nia ya kufanya na utafanikiwa hivyo hutaki kusikia maneno ya namna hiyo tena.
Kuwa na malengo yako mwenyewe,fanyia kazi malengo yako kila siku,jenga ndoto zako wewe mwenyewe,kumbuka kuwa usipojenga ndoto zako mwenyewe ipo siku utaajiliwa ili kujenga ndoto za mtu mwingine.
2.THUBUTU
Ili uweze kutoboa hakuishii kuwa na lengo tu,kama ilivyo kwenye harakati za kutoboa kitu ni lazima kunakuwa na mfumo mzima wa utoboaji,utoboaji wa kwenye maisha unahitaji ujasiri mkubwa,unahitaji uthubutu wa mtu katika jambo ambalo analifanya.Hebu fikiria ndugu yangu kama Msanii Diamondi angekuwa anaimba nyumbani kwake akiwaimbia kaka na dada zake bila kuthubutu kuingia studio na kurekodi na kujitangaza Je leo tungemjua?
Kudhubutu ni kitu/kifaa muhimu sana ambacho kila anayetaka kutoboa anatakiwa kuwa nacho.Watu wengi wanashindwa kufikia malengo yao kwa sababu ya kukosa kifaa hiki kinachoitwa uthubutu.Kama utapanga malengo makubwa na kuweka mikakati jinsi ya kufikia malengo yako lakini bila uthubutu wa kufanya itakuwa ni kazi bure.
Uthubutu ni hatua muhimu sana sababu inaweza kutengeneza nadharia ya lengo lako kwenda kwenye uhalisia,na hapa ndipo unapoanza kutengeneza ndoto yako.
Katika kutekeleza kipengele hiki utakutana na mambo mengi,watu wa kila aina wenye kukutia moyo na kukuvunja moyo,lakini nikutie moyo msomaji wangu kuwa fanya kile ulichodhamilia kufanya bila kuvunja sheria za nchi yako.
3. TENGENEZA MTANDAO
Ninapozungumzia mtandao sizungumzii mtandao wa simu za mkononi au mezani,bali nazungumzia mtandao wa watu ambao wanaweza kukusapoti au kukushika mkono katika kazi yako.
Mtandao huu unaweza kuwa ni muunganiko wa watu wako wa karibu,shabiki wa kazi yako au watu walio na uwezo wa kukuvusha hapo ulipo na kwenda katika hatua nyingine.Mfano wa mtandao ambao unaweza kuutengeneza ni huu hapa, Wewe ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za injili,una mashabiki wa kutosha kwa sababu ya nyimbo zako za kuvutia na zenye kusisimua ,pamoja kuwa ni mwimbaji mzuri wa nyimbo hizo hauna pesa za kulipia gharama za kurekodi.
Jambo la kwanza anza kuwajua mashabiki wako ni kina nani,nyadhifa zao pengine na hata karama zao juu ya utoaji.Tengeneza orodha ya mashabiki wako ambao wanaweza kukusapoti,pia tengeneza orodha ya mashabiki ambao wanaweza kukutangaza kwa watu wengine ili uendelee kukuza mtandao wako.
Hakuna biashara,kipaji kilichoweza kufanikiwa bila ya kuwa na mtandao wa watu,kumbuka kuwa mtandao huu umebeba utajiri wako(mafanikio yako) ya kile unachofanya.
4.JIAMINI MWENYEWE
Hii ni siri kubwa ambayo watu wengi hawana,wengi wamekuwa waoga kuanzisha kitu fulani ambacho unakiamini kuwa kitaweza kukuletea matokeo chanya katika maisha yako(kutoboa).Usifikirie wala usijali maneno ya watu ambayo yanakukatisha tamaa,fanya bila kujali watu watazungumza nini juu yako.
Jaribu kujilinganisha na mtu wako wa kuigwa na jenga picha katika akili yako jinsi ambavyo unavyotaka kuwa.Mfano unataka kufungua kampuni kubwa,tengeneza picha ya kampuni hiyo katika akili yako kwanza,jaribu kujiona kuwa wewe ndio mkurugenzi wa kampuni hiyo,siku zote mafanikio huanzia kwenye ndoto.
5. JIFUNZE KILA SIKU.
Wahenga walisema "Elimu haina mwisho",msemo huu unaenda sambamba na siri ya mafanikio kwani ni lazima uwe mtu wa kujifunza kila siku kupitia vitabu,magazeti na mitandao ya kijamii.
Hakuna aliyeweza kufanikiwa pasipo kujifunza kwa kusoma,kuhudhuria semina za ujasiliamali au kubadilisha mawazo/uzoefu wa jambo fulani.Kutoboa sio lelemama bali unatakiwa kukaza buti pasipo kulegeza,kutoboa huanza na hatua ndogo sana moja ya hatua hizo ndogo ni hizi za kujifunza kila siku,sababu ya kujifunza kila siku ni kwamba,dunia inabadilika kila kukicha,kumekuwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yanakua kwa spidi kubwa sana kiasi kwamba kama hautawekeza muda wako kwenye kujifunza kila siku utabakia na teknolojia ya mwaka 47.
6. FANYA PASIPO KAWAIDA
Ili uweze kutoboa ukuta unahitaji nguvu na akili kubwa,kwani ukitoboa vibaya unaweza ukaangukiwa na ukuta,umakini wako uwe sambamba na kuvunja rekodi za dunia ambazo ziliwahi kuwekwa katika kazi au kipaji ulichonacho.
Na ukitaka kutoboa vizuri usiige staili kwani,watu wamezoea kufanya mambo kawaida,hasa kuiga kutoka kwa mtu fulani,kampuni fulani,shirika fulani.Jaribu kuwa mbunifu katika biashara yako au kazi yako,mafanikio makubwa huletwa na ubunifu ambao utaishangaza duania.
7.USIOGOPE KUSHINDWA
Hebu fikiria juu ya hili,kama mgunduzi wa ndege angeogopa kufanya majaribio ya kurusha ndege fikiria dunia ingekuaje?Au kama watafiti wa dawa wangeogopa kutafiti tiba za magonjwa mbalimbali Je dunia ingekuwa katika hali gani?
Usiogope kufanya jambo ambalo liko katika malengo yako,tambua ya kuwa kadri unavyofanya majaribio mengi zaidi jua ya kuwa kushindwa kuko mbele yako,unaweza ukakutana na vikwazo vingi ambavyo vitakukatisha tamaa usiogope,hata kama ukianguka simama pukuta mavumbi na kusonga mbele kumbuka ya kuwa huwezi kuwa mshindi siku zote bila ya kuwa na maumivu.
Ukiogopa kushindwa ujue ya kuwa huwezi kujisimamia/kujiendesha mwenyewe,unajiendesha mwenyewe kwa sababu unaamini katika ndoto zako na unaamini kuwa upo sahihi kwa kila unalolifanya na unaamini kuwa ipo siku utatoboa tu.
8. USISIKILIZE KWA WALIOSHINDWA
Ni mara ngapi umesikia huwezi kufanya hili,huwezi kufanya vile kwa sababu haijawahi kufanywa?Ni mara ngapi umesikia huwezi kufanya hili kwa sababu mimi nilishindwa/mtu flani alishindwa?Binafsi napenda kuambiwa hivyo ili niwe wa kwanza kufanya na kuwaaminisha watu kuwa kitu hicho kinawezekana kufanywa.
Mfano nilipokiwa chuoni,marafiki zangu walinibeza na kuniambia kuwa siwezi kuandika kitabu na kukisambaza Tanzania nzima kwa sababu ya ukosefu wa fedha,niliamua kutafuta pesa kwa udi na uvumba,nikawa mwandishi wa kujitolea katika gazeti flani,baada ya miezi 9 nilipata pesa ya kuchapisha kitabu cha kwanza kopi 4,000 na kusambaza Tanzania nzima.Je kama ningesikiliza maneno ya watu hawa ningeweza kufanya hivyo?Ukitaka kutoboa usiangalie ugumu wa unachokitoboa wala ubutu wa kifaa unachotobolea unachotakiwa kufanya ni kuangalia namna gani unaweza kubadili ugumu wa jambo kuwa fulsa.
9.FANYA KAZI KWA BIDII
Watu wengi hukosa ufanisi wa kazi zao kwa kushindwa kufanya kazi kwa bidii,amka asubuhi na mapema ikiwezekana saa 11 alfajili hii itakusaidia wewe kupanga siku yako vizuri,anza na mambo ambayo wewe umejiwekea kuyafanya kila siku Mfano.Mimi kila siku asubuhi naandika kurasa mbili za hadithi kisha naendelea na shughuli zingine,hii inanisaidia kuendeleza kipaji changu na kuweza kufikiri zaidi.Hata wewe nakushauri kama unaweza jitahidi kila siku asubuhi tunga na uandike ujumbe mfupi wa maneno wa kutiana moyo tuma kwenye group la whatsap au mtumie rafiki yako hii itaksaidia sana.
Bila kufanya kazi kwa bidii kutoboa utakusikia kwa jirani yako tu,hakuna aliyewahi kuwa tajiri ili hali ni mzembe kazini,hakuna aliyewahi kufanikiwa ili hali anaamka saa 04:00 ausubuhi.Mo Dewji ni mmoja kati ya vijana matajiri zaidi Duniani lakini Mo amekuwa akiamka asubuhi saa 10:00 jioni na kuanza maandalizi ya kwenda ofsini kwake.Kama tajiri mkubwa kama huyu anaamka alfajiri,vipi wewe ambaye haumiliki hata kipande cha ardhi?
10. SAIDIA WATU
Kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali ni kitu kizuri katika maisha ya kila siku,msaada hukuwezesha wewe kufungua milango yako ya mafanikio,sio lazima kusaidia kwa kutoa pesa unaweza kusaidia watu kwa kuwashauri vizuri,kuandika makala nzuri kama hii au kuwatamkia maneno mazuri ya kuwatia moyo na kuwa bariki.
Ni mimi mwandishi wako Bundala Izengo 0656669989

Comments
Post a Comment